TAIFA STARS YAFUFUA MATUMAINI YA KUFUZU AFCON BAADA YA KUICHAPA ETHIOPIA 2-0
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeweka hai matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Ethiopia leo katika mchezo wa Kundi H Uwanja wa Stade des Martyrs, Jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mabao ya Taifa Stars yamefungwa na mshambuliaji wa Al-Talaba ya Iraq, Simon Happygod Msuva dakika ya 15 na kiungo wa Azam FC ya nyumbani, Dar es Salaam, Feisal Salum Abdallah dakika ya 31.
Kwa ushindi huo, Taifa Stars inafikisha pointi saba katika mchezo wa tano na kurejea nafasi ya pili ikiizidi pointi moja Guinea, ambayo hata hivyo ina mechi moja mkononi inacheza na DRC usiku huu Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara Jijini Abidjan nchini Ivory Coast.
DRC ambao wamekwishafuzu baada kwa pointi zao 12 katika mechi nne za awali wanaongoza Kundi H, wakati Ethiopia yenye pointi moja katika michezo mitano inashika mkia.
Taifa Stars inarejea usiku huu kwa ndege maalum waliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kujipanga kwa mchezo wa mwisho wa Kundi H Kufuzu AFCON dhidi ya Guinea Jumanne ya Novemba 19 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment