ATEBA APIGA MBILI SIMBA SC YAITANDIKA TABORA UNITED 3-0


TIMU ya Simba SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji, Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Chachu ya ushindi wa leo ni winga Mkongo, Elie Mpanzu Kibisawala aliyesaidia upatikanaji wa mabao yote, mawili yakifungwa na mshambuliaji Mcameroon, Leonel Christian Ateba Mbida na lingine beki, Shomari Salum Kapombe.
Bao la kwanza Ateba alipokea pasi ya Mpanzu na kufunga dakika ya 12 na la pili akafunga kwa penalti dakika ya 34 kufuatia Mkongo huyo kuangushwa na beki Mkongo-Brazzaville, Faria Jobel Ondongo. 
Bao la tatu Ateba alipokea pasi ya Mpanzu tena akiwa kwenye nafasi ya kufunga, lakini akamsetia Kapombe aliyekuwa anatokea nyuma  na kufumua shuti lililotinga nyavuni.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 43 na kurejea kileleni ikiwazidi pointi moja mabingwa watetezi, Yanga baada ya wote kucheza mechi 16.
Tabora United kwa upande wao wanabaki na pointi zao 25 za mechi 16 pia nafasi ya tano.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA