SIMBA SC YAWAPIGA TMA STARS 3-0 NA KUTINGA 16 BORA KOMBE LA CRDB
TIMU ya Simba imefanikiwa kuingia Hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TMA Stars ya Arusha leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC katika mchezo huo wa mkondo mmoja wa Hatua ya 32 Bora Kombe la CRDB yamefungwa na beki Mburkinabe, Valentin Nouma dakika ya 17, mshambuliaji Sixtus Robert Sabilo aliyejifunga dakika ya 19 na mshambuliaji Mcameroon, Christian Leonel Ateba Mbida dakika ya 76.
Simba SC sasa itakutana na Big Man FC ya Tanga iliyoitoa Tanzania Prisons kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1 Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Ikumbukwe jana Fountain Gate iliingia kwenye orodha ya timu za Ligi Kuu zilitupwa nje na timu za madaraja ya chini katika hatua hii baada ya kutolewa na Stand United kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya kufungana bao 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.
Timu nyingine za Ligi Kuu zilizoga michuano hii ni Azam FC iliyotolewa na Mbeya City kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, Dodoma Jiji iliyotolewa na Leo Tena ya Kagera kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 1-1 Jijini Dodoma katika Hatua ya Timu 64 na Prisons iliyotolewa na Big Man.
Comments
Post a Comment