AZAM FC YATINGA FAINALI KOMBE LA MUUNGANO
TIMU ya Azam FC imefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Muungano baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMKM jioni ya leo Uwanja wa Gombani, Pemba.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, beki na Nahodha Lusajo Elukaga Mwaikenda dakika ya 63 na sasa Azam FC watakutana na JKU katika Nusu Fainali.
Mchezo uliotangulia wa Robo Fainali jioni ya leo Zimamoto iliifunga Coastao Union 1-0 hapo hapo Uwanja wa Gombani na sasa itakutana na mshindi wa Robo Fainali ya mwisho kati ya Yanga na KVZ zitakazomenyana kesho kuanzia Saa 1:15 usiku hapo hapo Gombani.
Mechi za Nusu Fainali ya michuano hiyo maalum ya kuazimisha sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania tukufu Aprili 26, mwaka 1964 zitafuatia Aprili 28 na 29, wakati Fainali itachezwa Mei 1 hapo hapo Uwanja wa Gombani.
Mabingwa watetezi, Simba wameshindwa kushiriki michuano ya mwaka huu kwa sababu wanakabiliwa na mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kesho Jijini Durban.
Simba SC ilitwaa taji la michuano hiyo iliyoanza mwaka jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, bao pekee la kiungo Msenegal, Babacar Sarr, dakika ya 77.
Sarr alifunga bao hilo akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Israel Patrick Mwenda kufuatia mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Simba SC ilizawadiwa Sh. Milioni 50, wakati washindi wa pili, Azam FC walipata Sh. Milioni 30.
Comments
Post a Comment