YANGA NAO WAINGIA FAINALI KWA MATUTA PEMBA
MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC wamefanikiwa kuingia Fainali ya Kombe la Muungano baada ya ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Zimamoto kufuatia sare ya kufungana 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Gombani, Pemba.
Shujaa wa Yanga leo ni kipa Abdultwalib Hamidu Mshery aliyeokoa penalti za wachezaji wawili wa Zimamoto, Said Mwinyi na
Suleiman Said, huku ya Yussuf Idrisa ilkigonga mwamba na ya Abdulhamid Ramadhan pekee ndiyo ilimpita na kutinga nyavuni.
Waliofunga penalti za Yanga ni mabeki Israel Patrick Mwenda na Bakari Nondo Mwamnyeto na mshambuliaji Clement Francis Mzize huku ya Maxi Mpia Nzengeli pekee ikienda nje.
Katika dakika 90 za mchezo, Yanga walitangulia kupata bao kupitia kwa kiungo Mkongo, Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 29, kabla ya Said Mwinyi kuisawazishia Zimamoto kwa penalti dakika ya 71.
Fainali ya michuano hiyo maalum ya kuazimisha sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania tukufu Aprili 26 itachezwa Mei 1 hapo hapo Uwanja wa Gombani — na Yanga itakutana na JKU iliyoitoa Azam FC kwa kuichapa mabao 2-1 hapo hapo Gombani.
Mabingwa watetezi, Simba wameshindwa kushiriki michuano ya mwaka huu kwa sababu wanakabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba SC ilitwaa taji la michuano hiyo iliyoanza mwaka jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, bao pekee la kiungo Msenegal, Babacar Sarr, dakika ya 77.
Sarr alifunga bao hilo akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Israel Patrick Mwenda kufuatia mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Simba SC ilizawadiwa Sh. Milioni 50, wakati washindi wa pili, Azam FC walipata Sh. Milioni 30.
Comments
Post a Comment