ZIMAMOTO YAIREJESHA TANGA COASTAL UNION MAPEMA TU


TIMU ya Zimamoto imefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Muungano baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastao Union ya Tanga jioni ya leo Uwanja wa Gombani, Pemba.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Rashid Salum dakika ya 28 na sasa wanaungana na ndugu zao, JKU waliokuwa wa kwanza kutinga Nusu Fainali jana jioni kwa ushindi wa penalti 6-5 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika ya 90 hapo hapo Uwanja wa Gombani, Pemba.
Baadaye kuanzia Saa 1:15 usiku wa leo KMKM watacheza Azam FC ya Dar es Salaam katika Robo Fainali ya tatu ya michuano hiyo usiku hapo hapo Uwanja wa Gombani.
Vigogo, Yanga watakamilisha hatua hiyo ya Robo Fainali ya michuano hiyo maalum ya kuazimisha sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania tukufu Aprili 26, mwaka 1964 — kwa kumenyana na wenyeji wengine, KVZ kuanzia Saa 1:15 usiku.
Mechi za Nusu Fainali zitafuatia Aprili 28 na 29, wakati Fainali itachezwa Mei 1 hapo hapo Uwanja wa Gombani.
Mabingwa watetezi, Simba wameshindwa kushiriki michuano ya mwaka huu kwa sababu wanakabiliwa na mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kesho Jijini Durban.
Simba SC ilitwaa taji la michuano hiyo iliyoanza mwaka jana kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, bao pekee la kiungo Msenegal, Babacar Sarr, dakika ya 77.
Sarr alifunga bao hilo akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Israel Patrick Mwenda kufuatia mshambuliaji Mcameroon, Leandre Willy Essomba Onana kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Simba SC ilizawadiwa Sh. Milioni 50, wakati washindi wa pili, Azam FC walipata Sh. Milioni 30. 


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA