SERIKALI YAZIAGIZA BMT NA TFF ZIHAKIKISHE UCHAGUZI YANGA UNAFANYIKA NDANI YA SIKU 30

Na Shamimu Nyaki –WHUSM
SERIKALI imeliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha uchaguzi wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam unafanyika ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo katika mkutano na Waandishi wa Habari jana mjini Dodoma ambapo amesema kuwa migogoro iliyokuwepo huko nyuma imeshafika tamati hivyo uchaguzi ndani ya Klabu hiyo ni lazima ufanyike.
“Nailekeza BMT iwaelekeze TFF kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa na uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans unafayika ndani ya siku 30 kuanzia sasa,” alisema Singo.


Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari jana mjini Dodoma uchaguzi wa Yanga. Kulia ni Katibu Mtendaji wa BMT, Alex Nkenyenge.


Aidha, Singo amewasihi Viongozi, wanachama na wapenzi wa Yanga kutoanzisha migogoro wala vikwazo vingine bali kutumia siku 30 hizo kufanya uchaguzi ili kupata viongozi watakaoisimamia na kuiongoza Klabu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BMT, Alex Nkenyenge amesema amepokea maagizo hayo na atayafanyia kazi mara moja ili kipindi kilichowekwa na Serikali cha siku 30 Klabu ya Yanga iwe tayari ina uongozi.
Nkenyenge ameongeza kwamba atahakikisha Kamati ya Uchaguzi ya TFF inapanga utaratibu unaotakiwa kufuatwa kulingana na Katiba ya shirikisho hilo ili uchaguzi huo ufanyike hatimaye migogoro iliyodumu kwa muda mrefu ndani ya Klabu hiyo ifikie mwisho na Klabu iendelee kufanya vizuri katika mpira wa miguu.
Yanga ya Dar es Salaam ni miongoni mwa klabu kubwa za mpira wa miguu hapa nchini ambayo kwa muda mrefu haijatekekeleza uchaguzi kwa mujibu wa Katiba yao. 


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA