MAREFA WATANO KUCHEZESHA FAINALI ASFC AZAM FC NA LIPULI KESHO UWANJA WA ILULU

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemtangaza Hance Mabena (pichani) kutoka Tanga kuwa mwamuzi wa mchezo wa fainali ya Kombe la shirikisho la hilo, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) utakaopigwa kesho Jumamosi Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
Katika mchezo huo watatumika waamuzi sita kwa mara ya kwanza kwenye historia ya soka la Tanzania ambapo Mabena atasaidiwa na jumla ya waamuzi watano, wawili wa pembeni, wawili wa kwenye magoli na mmoja wa akiba.
Mfumo wa kuwa na waamuzi sita ulianza kutumiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwenye AFCON ya vijana chini ya miaka 17 iliyofanyika nchini mwezi Aprili 2019.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyotolewa leo, Hance Mabena atasaidiwa na Mohamed Mkono kutoka Tanga kama mwamuzi msaidizi namba moja, Frednarnd Chacha kutoka Mwanza kama mwamuzi msaidizi namba 2, na Abubakar Mturo kutoka Mtwara atakuwa ni mwamuzi wa akiba.
Waamuzi wasaidizi walioteuliwa kukaa kwenye magoli ni Martin Sanya kutoka Morogoro na Florentina Zablon kutoka Dodoma huku mtathmini wa waamuzi akiwa ni Lesile Liunda kutoka Dar es Salaam na kamishna wa mchezo ni Salum Kurunge kutoka Geita. .
Fainali hiyo ya kukata na shoka, itawakutanisha wababe wawili wa michuano hiyo msimu huu, Azam FC kutoka Dar es Salaam, na Lipuli FC kutoka mkoani Iringa kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi kuanzia saa 9:00 Alasiri na kukufikia mbashara kupitia #AzamSports2.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA