YANGA SC YAWAFUATA PYRAMIDS FC KIKAMILIFU KUJARIBU KUPINDUA MEZA CAIRO JUMAPILI

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KIKOSI cha Yanga SC kimeondoka leo jioni mjini Dar es Salaam kwenda Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano, mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Pyramids FC Jumapili wiki hii Uwanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 mjini Cairo.
Yanga SC inatakiwa kushinda 2-0 ugenini au kushinda kwa tofauti ya bao moja kuanzia 3-2 kwenye mchezo huo utakaoanza Saa 4:00 usiku, kufuatia kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Huo ulikuwa mwendelezo wa rekodi ya Yanga kutoshinda nyumbani mechi za michuano ya Afrika kuanzia Ligi ya Mabingwa ambako ushindi wa ugenini wa 1-0 uliwavusha Raundi ya pili baada ye sare ya 1-1 nyumbani na Township Rollers kabla ya kwenda kutolewa na Zesco United kufuatia kufungwa 2-1 Ndola ikitoka kutoka sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Na pamoja na kuuhamishia Mwanza mchezo wake na Pyramids FC kwa imani ya kupata ushindi, lakini mambo yalikuwa magumu zaidi baada ya kufungwa kutoka sare za Dar es Salaam.   
Jumapili mabao ya Pyramids FC yalifungwa na kiungo Mburkinabe, Eric Traore dakika ya 42 na beki Omar Gaber dakika ya 63  wote walimalizia krosi za mshambuliaji Mohamed Farouk, wakati bao pekee la Yanga lilifungwa na kiungo wake, Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Na siku hiyo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mkongo, Mwinyi Zahera, ilimaliza pungufu baada ya beki wake mzoefu, Kelvin Yondan kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 90 na ushei.
Wachezaji walioondoka leo jioni kwenda Misri ni makipa; Farouk Shikalo, Metacha Mnata na Ramadhani Kabwili na mabeki; Juma Abdul, Muharami Issa ‘Marcelo’, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro na Ally Ally.
Viungo ni Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Papy Kabamba Tshishimbi, Jaffar Mohamed, Raphael Daudi, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Patrick Sibomana, Issa Bigirimana na Mapinduzi Balama, wakati washambuliaji ni Juma Balinya na Sadney Urikhob.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA