WAZIRI DK. NDUMBARO ATEMBELEA MAKAO MAKUU YA CAF NA KUZUNGUMZA NA KATIBU MKUU
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amefanya ziara katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Cairo nchini Misri.
Dk. Ndumbaro amefanya ziara hiyo Septemba 25, 2023 ambapo amekutana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Veron Mosengo-Omba na wamejadili masuala mbalimbali ya kuboresha mchezo wa soka nchini.
Waziri Dk. Ndumabaro katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia pamoja na watumishi kutoka wizara hiyo na TFF.
Katika hatua nyingine, Waziri Dk. Ndumbaro ameongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea Ubalozi Cairo nchini Misri kabla ya siku ya kupiga kura ya kupata nchi mwenyeji wa Mashindano ya Afrika (AFCON 2027) itakayopigwa Septemba 27, 2023 nchini humo.
Ndumbaro amesema Tanzania, Kenya na Uganda kupitia Marais wa nchi hizo wako tayari kwa ajili ya mashindano hayo kwa kuwa zina mazingira mazuri ikiwemo miundombinu ya michezo ambayo ipo na inakidhi mashindano hayo, usafiri na malazi ya kutosha katika nchi hizo unaochagizwa na maeneo mazuri ya Utalii.
Naye Balozi wa Tanzania nchini humo, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema atahakikisha anawashawishi Mabalozi wa nchi mbalimbali kuunga mkono fursa hiyo adhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Wallace Karia amesema nchi hizo zinayo nafasi ya kushinda kwakua hazijawahi kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ambapo amesema viwanja tisa vitatumika katika nchi hizo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amesema wanaendelea kushirikiana na wajumbe watakaopiga kura ili kuzipa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki nafasi ya kuandaa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa michuano hiyo mwaka 1957.
Tanzania, Kenya na Uganda zimeungana kupitia maombi ya EA Pamoja Bid 2027 ili kutimiza azma ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa Afrika.
Comments
Post a Comment