SERIKALI YATUMIA BILIONI 2.4 KUGHARAMIA TIMU ZA TAIFA
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Februari, 2024 Wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 2.4 kugharamia Timu mbalimbali za Taifa katika mashindano ndani na nje ya nchi.
Amesema hayo wakati akiwasilisha utekekezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2023/24 na Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 24/25 kwenye Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo leo Machi 22, 2024 Bungeni Jijini Dodoma.
Amezitaja baadhi ya timu hizo kuwa ni Timu ya Taifa ya ya Gofu Wanawake iliyoshiriki mashindano ya Gofu Afrika Mashariki na Kati nchini Rwanda mwezi Novemba na kuwa mshindi wa kwanza, Timu ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars) ambayo iliwezeshwa kushiriki michuano ya kufuzu kucheza WAFCON yanayotarajiwa kufanyika Juni, 2024 nchini Morocco, kuwezesha Timu nane ikiwemo Judo, Riadha, Mpira wa Miguu Wanawake, ngumi kriketi wanaume na Wanawake kushindana mashindano ya Michezo Afrika (All African Games) yanayoendelea nchini Ghana ambapo hadi sasa medali mbili za mchezo wa ngumi zimepatikana.
Mafaniko mengine ambayo ameyataja Mhe. Waziri ni kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo hadi Februari 2024, Wizara kwa kushirikiana na Benki za CRDB na NBC imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.2 kwa miradi 216 katika Halmashauri 31 za mikoa 16 ya Tanzania Bara.
"Kwa kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Februari 2024 Wizara imetumia takriban Bilioni 10.17 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa eneo changamani la michezo, ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa,ujenzi wa vituo vya mazoezi na kupumzikia Dodoma na Dar es Salaam na ujenzi hosteli za Chuo Cha Michezo Malya ambao unaendelea" amesema Dk. Ndumbaro.
Katika Mpango wa Bajeti ujao Dk. Ndumbaro ameeleza kuwa, Wizara pamoja na Taasisi zake imepanga kutekeleza miradi 15 yenye thamani ya Bilioni 258 ikiwemo ujenzi wa ukumbi wa wazi wa Sanaa, Ukarabati wa Chuo Cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, ujenzi wa Akademia ya Michezo Malya, ujenzi wa eneo changamani la michezo Dodoma.
Comments
Post a Comment