SIMBA SC YASAJILI BEKI WA KULIA HODARI KELVIN KIJIRI
KLABU ya Simba imemtambulisha beki wa kulia, Kelvin Sospeter Kijiri (24) kutoka Singida Big Stars kuwa mchezaji wake kuelekea msimu ujao.
Beki huyo aliyeibukia KMC mwaka 2019, kabla ya kuhamia Singida Big Stars mwaka jana anakuwa mchezaji mpya wa 13 kwenye kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Wachezaji wengine wapya Simba ni pamoja na mabeki, Mburkinabe Valentin Nouma (24) kutoka FC Saint-Éloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wazawa, Abdulrazack Mohamed Hamza (21) kutoka SuperSport United ya Afrika Kusini na Lameck Elias Lawi (18) kutoka Coastal Union.
Wengine ni viungo, Mnigeria, Augustine Okejepha (20) kutoka Rivers United ya kwao, Port Harcourt, Omary Abdallah Omary (23) kutoka Mashujaa FC ya Kigoma, Yusuph Ally Kagoma (28) kutoka Singida Big Stars, Mzambia, Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya kwao, Kitwe, Débora Fernandes Mavambo (24) mwenye uraia pacha wa Kongo - Brazzaville na Angola kutoka Mutondo Stars ya Zambia.
Kuna washambuliaji pia, Mganda, Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua (22) kutoka Stella Club d'Adjamé ya kwao, Abidjan na mzawa, Valentino Mashaka Kusengama (22) kutoka Geita Gold.
Simba SC pia imeleta Kocha Mkuu mpya, Fadluraghman ‘Fadlu’ Davids (43) raia wa Afrika Kusini kuwa Kocha wake mpya Mkuu, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchika aliyeondoka April 28, mwaka huu.
Fadlu Davids amekuja na safu yake nzima ya Wasaisizi, wote raia wenzake wa Afrika Kusini, Kocha Msaidizi, Darian Wilken, Kocha wa Makipa, Wayne Sandilands, Kocha wa Fitness, Riedoh Berdien na Mchambuzi, Mueez Kajee.
Kikosi cha Simba SC kwa sasa kipo mjini Ismailia nchini Misri ambako kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya.
Comments
Post a Comment