MSUVA AIPELEKA TAIFA STARS AFCON 2025


HATIMAYE Tanzania imefanikiwa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwakani nchini Morocco baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea katika mchezo wa Kundi H Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji wa Al Talaba ya Iraq, Simon Happygod Msuva dakika ya 61 akimalizia pasi nzuri ya kiungo wa Yanga ya nyumbani, Dar es Salaam, Mudathir Yahya Abbas. 
Kwa ushindi huo, Taifa Stars inafikisha pointi 10 baada ya mechi zote sita za kundi hilo na kuungana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yenye pointi 12 za mechi tano kufuzu AFCON ya mwakani.
Guinea inabaki na pointi zake tisa baada ya mechi zote sita za kundi katika nafasi ya tatu, mbele ya Ethiopia yenye pointi moja katika mechi tano. 
Mechi ya mwisho ya Kundi H DRC wanamenyana na Ethiopia tangu Saa 1:00 usiku Uwanja wa Martyrs de la PentecĂ´te Jijini Kinshasa.
Hii inakuwa mara ya nne kihistoria Tanzania kufuzu AFCON baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 Misri na 2023 nchini Ivory Coast na mara ya kwanza kufuzu Fainali mbili mfululizo.
Ikumbukwe kwa tiketi ya uenyeji wakishirikiana na Kenya na Uganda – Tanzania pia watacheza Fainali za AFCON za mwaka 2027.


Comments

Popular posts from this blog

NYOTA WA KIKOSI CHA SIMBA KILICHOFIKA FAINALI KOMBE LA CAF 1993, DAMIAN KIMTI AFARIKI DUNIA