Posts

Showing posts from December, 2024

MJUMBE BODI YA WAKURUGENZI AZAM FC AFIWA NA BABA YAKE MZAZI

Image
MJUMBE was Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC, Careen Bahadour amefiwa na baba yake mzazi, Mzee Marhun Shermohamed 'Sheru' jana Jumatatu nchini Afrika Kusini alipokuwa anafanyiwa matibabu. Taarifa ya Azam FC mapema leo umesema kwamba mazishi yanafanyika Saa 4:00 asubuhi ya leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam baada ya Sala itakayofanyika msikiti wa Maamur, Upanga, “Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia ya @careem99_, ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huu,”imesema taarifa ya Azam FC mapema leo. Inna Lillahi Wainna Ilaihi Rajiun! 🙏🙏🙏

COASTAL UNION YAWACHAPA TANZANIA PRISONS MABAO 2-1 ARUSHA

Image
  BAO la dakika ya 90‘+5 la mshambuliaji Maulid Shaaban limeipa Coastal Union ushindi wa 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara mchana wa leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha. Katika mchezo huo ulioanza Saa 7:00 mchana wa leo baada ya kuahirishwa jana kutokana na mvua iliyoharibu mandhari ya Uwanja jana – Coastal Union walitangulia kwa bao la beki wa kushoto Mkongo, Hernest Briyock Malonga dakika ya 42 kwa penalti. Lakini mshambuliaji mzawa, Meshack Abraham Mwamita akaisawazishia Tanzania Prisons dakika ya 56 – lakini ndoto za Maafande kujapa pointi moja leo zikazimwa na Mau mtoto wa mzee wa Shebby. Kwa ushindi huo, Coastal Union wanafikisha pointi 16 katika mchezo wa 13 na kusogea nafasi ya tisa, wakati Tanzania Prisons inabaki na pointi zake 10 za mechi 12 sasa nafasi ya 13.

AZAM FC YAITANDIKA DODOMA JIJI 3-1 PALE PALE JAMHURI

Image
TIMU ya Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji, Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku wa jana Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. Mabao ya Azam FC yalifungwa na mshambuliaji Nassor Saadun Hamoud dakika ya 11, kiungo Feisal Salum Abdallah kwa penalti dakika ya 45’+3 na Dickson Mhilu aliyejifunga dakika ya 60, wakati bao pekee la Dodoma Jiji alijifunga pia beki Mkongo, Yanick Litombo Bangala dakika ya saba. Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 30 katika mchezo wa 13 na kurejea kileleni mbele ya Simba yenye pointi 28 na Yanga 27 baada ya wote kucheza mechi 11, wakati Dodoma Jiji inabaki na pointi zake 16 za mechi 13 pia nafasi ya tisa.

PAMBA JIJI YAILAMBA KEN GOLD KIDUDE KIRUMBA SHUGHULI YA MPOLE

Image
BAO pekee la mshambuliaji George Mpole Mwaigomole dakika ya 72 limeipa Pamba Jiji FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Ken Gold katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza. Kwa ushindi huo, Pamba Jiji inafikisha pointi 11 katika mchezo wa 13 na kusogea nafasi ya 13, wakati Ken Gold inaendelea kushika mkia kwenye ligi ya timu 16 ikibaki na pointi zake sita za mechi 13 pia. Mechi nyingine ya Ligi Kuu iliyopangwa kuchezwa jioni ya leo baina ya Coastal Union na Tanzania Prisons imeahirishwa kutokana na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kujaa maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jijini Arusha.